Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete amesema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015, chama chake kitaanguka vibaya.
Akaonya kuwa iwapo kitanusurika hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Aliyasema maneno hayo makali alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa,wilaya na wenyeviti wa wilaya zote wa chama hicho nchini mjini Dodoma hivi karibuni.
Ili kukisafisha chama hicho, Rais Kikwete amempa makamu wake, Phillip Japhet Mangula jukumu la kushughulikia viongozi wote wanaotuhumiwa kula rushwa.
Hiyo ni tahadhari iliyotolewa pia na mwanasiasa na kada mkongwe wa chama hicho Peter Kisumo hivi karibuni, akisema kuwa chama hicho kimenyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mbali na Kisumo, makada wakongwe wengine kama vile, Dk Hassy Kitine, Ibrahim Kaduma na Joseph Butiku nao walishaonya kuhusu jambo hilo.
Hata hivyo, nabaki najiuliza, Rais Kikwete naye atamlaumu nani katika suala hili?
Ninajiuliza hivyo kwa sababu Kikwete ndiye yuko madarakani na ana uwezo wote wa kupambana na rushwa, kwa nini asipambane ili kukinusuru chama chake?
Kikwete ni sawa na dereva anayejua gari linaelekea wapi anazo zana zote za kuhakikisha kuwa gari halipinduki. Sasa iweje gari likipinduka alaumiwe kondakta au utingo?
Anayo madaraka kama rais, ndiyo maana hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) inawajibika kwake, ni mwenyekiti wa baraza la mawaziri, anateua wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, mwanasheria mkuu wa serikali, wakuu wa mikoa na wilaya na watendaji wengineo.
Kwa madaraka yote hayo, Kikwete ameshindwaje kupambana na rushwa ndani ya chama wakati anazo sababu na uwezo wa kupambana na rushwa.
Kwa mfano, mwaka 2006, akiwa jijini Mwanza alikaririwa akisema kuwa anawajua wala rushwa, ila anawapa muda wajirekebishe. Je, wamejirekebisha au la au hakuna dhamira ya kuwaadhibu?Hata alipoingia madarakani miaka karibu minane iliyopita, tunaambiwa alikabidhiwa majira ya wauza dawa za kulevya na majambazi. Hadi leo hayaeleweki yaliishia wapi! Kikwete ndiye aliyeasisi mkakati wa kujivua gamba mwaka 2011 ukiwa na lengo la kukisafisha chama hicho ikiwa pamoja na kubadilisha sekretarieti yake. Kwa bahati mbaya, hadi leo hakuna aliyechukuliwa hatua kati ya watuhumiwa wengi wa ufisadi ndani ya chama hicho.
Halafu leo Kikwete anaibuka na kuonya kwamba chama hicho kitaanguka mwaka 2015 kama rushwa haitadhibitiwa.
Jiulize, nani aidhibiti rushwa ndani ya chama hiki na kwa vipi? Je, CCM ikianguka, nani alaumiwe? Tafakari.
Chanzo Gazeti la mwananchi
No comments:
Post a Comment