MKUTANO wa kujadili maendeleo ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, ulioitishwa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, jana uligeuka mwiba kwa mbunge huyo baada ya watu waliohudhuria kumtaka aeleze sababu ya kuwashambulia wapinzani wa chama chake katika majukwaa ya siasa badala ya kujikita katika kuhimiza maendeleo ya jimbo analoliongoza.
Mkutano huo uliopangwa kuanza saa nane kamili mchana ulilazimika kuanza saa 10 jioni, baada ya watu kutokujitokeza kama ilivyotarajiwa, ambapo hadi mwisho wa mkutano idadi ya watu waliohudhuria pamoja na waandishi wa habari walikuwa 42, huku zaidi ya viti 158 vilivyoandaliwa kwa ajili ya washiriki vikikosa wakaaji.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwigulu aliwatahadharisha wahudhuriaji kuweka masuala ya vyama pembeni na badala yake wajikite katika kujadili maendeleo ya Wilaya ya Iramba, ingawa alikuwa akiwahutubia waandishi wa habari ambao hawakuwa walengwa hasa wa mkutano huo.
Alisema kwa sasa vijana wengi wamepatwa na mfadhaiko kutokana na maisha kuwa magumu kunakochangiwa na kukosekana kwa ajira za uhakika, hivyo amejiandaa kuwa sehemu ya utatuzi wa tatizo hilo.
Alibainisha kuwa anatarajia kupeleka hoja binafsi bungeni itakayoitaka serikali kueleza kwa kina sababu ya vijana kukosa ajira licha ya kuwa na elimu ya ujuzi mbalimbali wanayoipata kutoka kwenye vyuo vilivyopo ndani na nje ya nchi kila mwaka.
Endapo Mwigulu atafanikisha kupeleka hoja hiyo ya ajira ya vijana itakuwa inafanana na ile iliyopelekwa katika vikao vya Bunge na Mbunge wa Nzega, Hamisi Kigwangala (CCM).
“Nitataka kupata takwimu sahihi ni vijana wangapi wamemaliza chuo na wangapi wameajiriwa serikalini au katika sekta binafsi na wangapi wamejiajiri au serikali ituambie kwanini vijana waliomaliza vyuo vikuu wanashindwa kujiajiri,” alisema Mwigulu.
Mmoja wa wananchi waliopata kuchangia mjadala huo wa maendeleo ya Wilaya ya Iramba, Elihuruma Himida, alisimama na kumueleza mbunge huyo aache kufanya siasa zisizokuwa na tija kwa Wanairamba, badala yake ajikite katika kuwaletea maendeleo aliyoahidi.
Himida alisema Iramba hakuna mabadiliko hususan katika Jimbo la Mwigulu na kwamba hakuna maji wala miundombinu itakayowawezesha wanafunzi kusoma vizuri.
“Tunataka maendeleo, maana si maneno ya kisiasa, kwetu elimu ni ya taabu, hatuna maji na hata suala zima la maendeleo kwetu ni ndoto, ninyi mnabaki kulumbana katika majukwaa ya kisiasa,” alisema mwananchi mwingine.